Tuesday 3 May 2016

UHURU WA VYOMBO VYA HABARI NA MINYORORO YA VIKWAZO!



Na Ally Mohammed Abdul-rahman,
Zanzibar, Tanzania,
Simu: + 255 655 572 594,
Barua-pepe, allymohammed01gmail.com

Leo, Jumanne, tarehe 03 Mei, ni Siku ya Uhuru wa vyombo vya habari Duniani, kwa muktadha wa neno "UHURU" linalenga kutoa nafasi, kutokuingiliwa, kutokupangiwa, kutokubugudhiwa na kila aina ya kuachwa kujiendesha ufanye kazi yako bila ya bugudha kutoka kwa mamlaka yeyote ilimradi sheria za nchi zinafuatwa.

Wakati tunasherehekea siku hii muhimu kwa taaluma yetu ni wazi kuwa tuna safari ndefu sana huko mbele, Uhuru wa Vyombo vya Habari 'umebakwa' na 'kunajisiwa' hadharani na wanasiasa, mamlaka za serikali, wamiliki wa vyombo vya habari, matajiri na hata baadhi ya taasisi zenyewe za habari.

Ndiyo! Umebakwa na kunajisiwa, tunahubiri kwenye vinywa na maandishi tu juu ya Uhuru wa Vyombo vya Habari lakini hatutendi vile tunavyohubiri katika vinywa vyetu.

Ni utamaduni wa kawaida kila ifikapo siku kama hii, wadau wa sekta ya habari nchini wakiongozwa na magwiji na wakongwe wenye uzoefu wa kushiba katika tasnia hii kukutana na kuangalia changamoto za tasnia na namna ya kuzishughulikia.

Mwaka huu Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari yanaadhimishwa kitaifa jijini Mwanza huku yakibebwa na kauli mbiu ya “KUPATA TAARIFA NI HAKI YAKO YA MSINGI, IDAI".

Maadhimisho haya yanafanyika kitaifa kwa mara ya nne na yanalenga kukumbusha umma na dunia kwa ujumla umuhimu wa vyombo vya habari, kufanya kazi yake bila kuingiliwa na mtu ama chombo chochote.

Zaidi ya wadau 250 wakihusisha waandishi wa habari wakongwe na wanaochipukia, wahariri, viongozi wa mashirika wahisani wa ndani na nje, wawakilishi wa mihimili ya nchi (Serikali, Bunge na Mahakama), wasomi wa vyuo vikuu na mabalozi mbalimbali wamekusanyika jijini Mwanza kwa ajili ya maadhimisho hayo ambayo kilele chake ni leo.

Ni hatua nzuri na kweli kuna baadhi ya mabadiliko yanaonekana kutokea kutokana na mikutano ya aina hiyo, lakini niseme bado changamoto zipo nyingi sana katika kupata uhuru wa vyombo vya habari kivitendo na sio porojo zisizokuwa na tija yeyote.

Yapo matukio kadhaa ambayo yanafanyika bila ya kificho kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari, matukio hayo yanafanywa na makundi niliyoyataja hapo juu.

Ni dhambi kitaaluma kwa mtu ambaye hana hata introduction (utangulizi) ya uandishi wa habari halafu eti anatoa maelekezo news room (chumba cha habari) habari gani iende na habari gani isiende kwa interests (matakwa) binafsi ambazo kimsingi zinaingilia uhuru wa habari.

• Kuna baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari wamechukuwa jukumu la kuwa wahariri kwenye 'media house' wakati hawana taaluma yeyote ya habari, hiki ni kiwango cha uzamivu (PhD) cha dharau.

• Wapo baadhi ya wanasiasa wamefanikiwa kupenya ndani ya vyombo vya habari na kuvimiliki kitaaluma wakati wenyewe hawana elimu yeyote inayohusu habari.

• Wapo matajiri wanaotumia fedha zao kulazimisha habari wanazozitaka wao, kama kuna habari za 'kuwabomoa' hata kama zipo kimaadili watatumia nguvu ya fedha zao kuizima habari hiyo kwa gharama yeyote.

• Zipo baadhi ya mamlaka za serikali ambazo kwa asilimia kubwa wao ni maadui wa Uhuru wa Vyombo vya Habari, hawataki hata kusikia hizo habari zinazohusu uhuru wa habari, ukiikosoa serikali hata pale ambapo unalazimika ukemee kwa misingi ile ile ya taaluma na utawala bora kama wanavyohubiri basi utageuka adui usie na kikomo na watakushughulikia kwa njia zote za haramu wanazozijua wao.

• Kuna hizi taasisi za habari mfano wa MCT na TEF, baadhi yao, narudi baadhi yao na sio miongoni mwa huo mfano wangu, zenyewe zimegeuka kuwa upande wa serikali hata pale zinapoona Uhuru wa Vyombo vya Habari 'unanyongwa', watakaa kimya kama hawapo, hata 'press releases' zitawashinda kisa, wapo chini ya 'kwapa' za serikali na wao wanalinda 'mkate' wa kila siku (unafiki uliopitiliza).

Changamoto ni nyingi na haziwezi kutatulika kirahisi kama hatujaunganisha nguvu na kuwa na sauti moja ya kuisimamia taaluma na kuacha 'kuabudu' wanasiasa na taasisi za serikali zinazotumia nguvu kubwa kuminya na kunyamazisha kabisa kitu kinachoitwa "Uhuru wa Vyombo vya Habari".



Ukiwasikiliza na matendo yao ni vitu vinavyokinzana, ndiyo msingi wa kusema wanayoyaandika na kuyatamka ni tofauti sana na matendo yao, kiufupi hawana nia njema na wala hawapo tayari kuona uhuru wa vyombo vya habari unapatikana.

Pengine kwa kuwa serikali na wao wanamiliki vyombo vya habari na kimsingi vyombo hivyo haviwezi kutoka nje ya sera za serikali na wakati mwengine baadhi yao vinatumika kueneza 'propaganda' pale ambapo
wangepaswa kuikosoa serikali na kuwaonesha njia sahihi ya kupita, lakini watapata wapi nguvu hiyo wakati wapo chini ya usimamizi wa serikali?.

Ingawa kimsingi vyombo hivi vinatakiwa viwe vya umma na sio kuwa upande wa serikali hata kwa machafu lakini ni kama tayari 'vimetekwa' na sio tu kuwa upande wa Serikali bali kuwa sehemu ya propaganda na kuwa wasaidizi wa chama tawala kwenye kampeni za uchaguzi.

Ni tofauti na mashirika ya umma ya habari ya mataifa mengine kama vile Afrika ya Kusini (SABC) au Uingereza (BBC) ambapo wao vyombo hivi vinahudumia umma na sio kuwa wasemaji wa serikali na kusifia kila kitu cha serikali huku wakitetea hata yasiyostahili kutetewa.

Changamoto za waandishi wa habari sitozigusa hapa maana nalo ni JIPU lililopiga rangi, nitatafuta nafasi nyengine kulitumbua hili.

Tuadhimishe Siku ya Uhuru wa Vyombo wa Habari tukijua tuna dhima ya kuyatekeleza kwa vitendo yale tunayoazimia katika vikao vyetu vya tathmini ya tasnia hii.

Haitoshi kuadhimisha kwa kula, kunywa, kupeana posho kubwa na kupiga picha nyingi za pamoja na mgeni rasmi kisha yale ambayo yanakwamishwa kuwepo kwa uhuru wa vyombo vya habari tukayapuuza na kuja kujikumbusha tena kwenye maadhimisho mengine mwakani.

Vyombo vya Habari vina nguvu kubwa kama tutashikamana kwa umoja wetu na nguvu ya kalamu zetu heshima yetu lazima itakuja kwa kiwango kinachokubalika, kinyume chake tutaendelea kudai uhuru wa vyombo vya habari kila siku na milele hatutaona mabadiliko kwa hili.

No comments: